Jump to content

Sha'iri la Makunganya

From Wikisource

> Main Page/Kiswahili

Sha'iri la Makunganya (1898)
by Mzee bin 'Ali bin Kidogo bin il-Qadiri
283012Sha'iri la Makunganya1898Mzee bin 'Ali bin Kidogo bin il-Qadiri


"Sha'iri la Makunganya"; mwenye kuandika Mzee bin 'Ali bin Kidogo bin il-Qadiri, Zanzibar


1-6

Bismillahi awali,
ya pili rahmani
nataka kutakallam,
na khabari kwapani
msishikwe na ghururi,
tafaddalini jamani

7—12

na shamba mtapandiwa
leo mnajuta nini
baa la kujitakia?
bass mwalimkisema
ashukapo Jerumani

13-19

Tutapigana jihadi
Kwa rehema ya mannani,
Jeremani akashuka
Akangia fordani.
Pasiwe mtu kujibu
Ikawa kutaka amani,
Leo mnajuta nini

20-26

Baa la kujitakia?
Mtawambia kwa yaqini
Niwape yangu moyoni
Nitasema kwa baini
Waliondoka mjini
Waliokwenda utamboni
Kilwa Kivinje mjini.

27-32

Ntawataja fursani
Waume wanao shani
Waliondoka mjini
Wakaingia sitimani
Watoto wa Kijerumani.
Ma'askari yaqini

33-38

Elfu na sabini:
Kuwataja sitaweza
Watu wote kujitengeza:
Amiri jeshi Raamza,
Ndiye aliye haziria.
Leo mnajuta nini?

39-45

Baa la kujitakia?
Wazungu thabiti mitima yao
Yalikuwa marudia.
Wala haina khofu
Kulla harubu kuingia
Na furaha kuwapata,
Shindo wakilisikia,

46-52

Na bunduki mikononi
Mji wakuwania.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Kwa kulla neno ntatia
Hapana lakubaqia:
Khabari ya Makunganya.

53-58

Sikizeni ntawambia:
Alianza upotovu
Kufanya mambo daifu
Na watu kuta'arifa
Kujifanya mtukufu,
kumbe kijitu daifu

59-64

Machoni ukimtokea;
Wenziwe akawaghuri
Pasiwe kufikiri;
Wakaingiwa na ghururi
Wakaja wakafa zuri
Hatta shahada kutoa.

65-72

Ukali wake kama ra'adi
Jerimani; hawarudi.
Huenenda kama jaradi
Hapo watapotokea.
Askari wa Jermani
Anavowapamba kwa shani
Viatu viko miguuni
Na mabete kiunoni

73-80

Burangiti mgongoni
Gisi wanavowalia
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Walipoazim vita
Kwa Makunganya kufika
Hatta walipomshika
Na watu kumi na sita:

81-89

Hapana pakutokea
Ote wakatiwa nyororo
Wakawa kama watoro
Zikawafa roho zao
Nafsi zao kupotea.
Watu waliposhikana
Vita vilipopigana
Mjini mwa Makunganya
Watu kujikimbilia

90-98

Watumwa kwa wangwana;
Hapana mtu kusema
Wote wana teketea
Watu wa Makunganya
Wamekufa kama panya
Gisi alivoingiliwa.
Boma lake likavunjwa
Watu yake wakanyongwa
Wakewe wakapotea

99-106

Naye tanzini kangia.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Kwa hesabu sitawesha
Wengine nitawabaqisha
Wote wakapigwa picha
Pasiwe kusalia,
Leo mnajuta nini,

107-114

Baa la kujitakia?
Khabari nitawapani
Walio ondoka mjini
Ma'adwi wa zamani
Waliokwenda Kilwa Kishwani
Kumondoa Sulutani
Yeye bwana Vismani
Na tena na Govmani.

115-121

Sitima iko tayari
Imekwisha jingilia
Wakenda wasimwone.
Maneno yao wasiseme
Wakawa kama wagane
Hapa walipo kukaa.
Damiri yao moyoni

122-128

Wampate Vismani
Bana mkubwa wa shani
Aqili nyingi kichwani
Mtoto wa Kijermani
Ememiliki Kivinji
Hatta Kilwa Kishwani
Tangu awali ya Lindi

129-136

Hatta Tanga Afrikani.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Ushahidi sijatoa
Sasa mnawayawaya - ;
Bandari Salama Ulaia
Uzuri wamebarabara
Jinsi ilivotulia.

137-144

Zimekwisha sifa zake
Visman peke yake
Wala hana mwenzi wake
Ambaye kumzidia.
Kwa kulla neno ntatia
Ni kama hapa Afrika
Wala hana mushirika
Sikizeni ntawambia:

145-153

Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Yeye mtu taratibu
Hakuumbwa na ghadabu
Ukimwona mwarabu
Machoni mtokea;
Ameumbwa na rehema
Amefanya mambo mema
Inchi zote kutengea

154-162

Ajua sana kusema
Kiswahili kumwelea.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Niwacheni nimsifu
Na yeye mtu nadifu
Na la tatu mtukufu
Roho yake hana khofu.
Tena mtu shuja'a

163-170

Jina lake tulijua:
Tangu pwani hatta bara
Hapo asiyo sikia.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Kaipanda Afirika
Tangu nyanza hatta nyika
Hapana asipofika

171-178

Barra yote kutembea.
Amezaliwa Berlina
Vismani mtu mwema
Anaye nyingi rehema
Watu wote wamjua
Khabari hio kufika,
Walipotaka kumshika
Mwaka u nussu kupita,

179-187

Hatta siku zikipita
Shauri akafanyiza
Na zana akatengeza;
Wakenda wakifunza.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Ushairi ntasema sana
Siku waliokutana
Visman na Makunganya.

188-196

Kwanza alimtukana
Na yeye kajinamia
Kumtukana machoni kwake
Makunganya na watu wake
Kamwambia: mwanamke.
Nani anayo kujua?
Akisema akapoa
Kitini kajikalia
Kaondoka bana Mayoa

197-204

Maneno akitongoa
Kizungu: hayakumwelea.
Nitawaambia kwa yaqini
Sahha na bana Feltini
Wakasema Kiswahili
Watu wote kusikia:
Bana Sahha kamwambia
Leo mnajuta nini,

205-212

Baa la kujitakia?
Banyani na Wahindi
Waarabu na Washihiri
Na wengine Waswahili
Wote wakaitikia.
Makunganya asiseme
Wakanyongwa watu saba
Na mwenyewe ndio wa nane,

213-221

Hapo asiotazama;
Watumwa na wangwana
Wakubwa hatta vijana
Wote wakashuhudia:
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Sahha ni bana mzuri
Wahindi akawashauri
Wote wakajikania.

222-230

Bana Sahha akafikiri
Aqili ikamwingia
Roho ikaghadhabika
Karakoni akafika
Askari akaweta
Wote wakamtokea;
Walingiwa na uchungu
Askari na wazungu
Wote wakamwandamia.

231-238

Akafanyiza nadhari
Akaweka watu wawili
Mzungu na Asikari
Nyumba moja kumngojea;
Maneno nitawakifu
Zikesha zote nyumba tatu
Na ya nnne ntawambia
Nyumba iliobaqia

239-246

Na jina utawatajia
Ya Muhindi Kassum Pira
Bana Sahha akaondoka
Ile nyumba akangia
Vitabu akavichukua
Mfukoni akavitia.
Akawashauri sana:
Wahindi wanne wakakana,

247-254

Bana Sahha akitongoa
Vitabu akavitoa:
Ote wakujinamia.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Twamjua ma'alum
Bana Sahha kwa hukum
Hukumu anaiweza

255-292

Shauri kuitengeza;
Naye kawatoza fedha
Wahindi kujitolea.
Na Wahindi Kilwa wengi
Wakatoa fedha nyingi.
Nitafanyiza hesabu
Halafu ntawambia:
Najua kwa yaqini

263-269

Ni elfu 'asherini
Hesabu nawambia
Ni watajiri mbali-mbali.
Niwasifu mahodari:
Abdallah bin Omari;
Ndiye aliyetokea,
Hakukaa mwanamke,

270-276

Hakungojea ashikwe,
Mwenyewe alijiendea
Hatta tanzini kufika
Na shingo akaipeleka
Na tanzi akajitia
Na watu kumtazama
Naye kimya hakusema

277-284

Marra akajangukia
Khabari nisha wapani
Ote meshasikia
Ya Makunganya kuuwawa
Miji yote wamejua
Mwanzo hatta akhiria:
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?

285-292

Wahindi wakatiwa nyororoni
Wakawekwa karakoni
Sitima wakangojea,
Ilipokuja wakapakiwa
Wote safiria.
Wakafika Bender-Essalama
Wote wkaonekana
Watumwa kwa wangwana

293-300

Wote wakatazama
Hapana asiwaone:
Wakashukwa kama watumwa
Kette ilivowangia.
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia?
Bana Sahha twamjua ma'alumu
Ajua sana hukumu

301-308

Kawafunga kwa siku zake
Aijua miaka yake,
Halafu atawafungua:
Hukum yao kabisa
Miaka saba ikafika
Wote watafunguliwa.
Wakapakiwa sitima ingine
Na kwao wasikuone

309-315

Wakawa kama wagane,
Tanga wakasikilia.
Wakatiwa katika kazi ya gari
Kufanyiza hawajui
Wahindi wanaolia.
Msimamizi tayari
Yupo kuwapokea

316-322

Machozi hujifutia
Kazi wakifanyia:
Leo mnajuta nini,
Baa la kujitakia
Qadi tamati sha'ri
Nimesha kuwapa khabari
Ya Kilwa iliyojiri

323-330

Yote nimeidhukuri
Sina nililoacha
Kwa khabari ya Makunganya
Kauwawa kimya-kimya
Fitina hapana tena
Kilwa yakutokea.
Nimefikiri peke yangu
Hatoa rohoni kwangu,

331-338

Mimi na bibi yangu
Nyumbani tumejikalia:
Nilipo nikiandika
Bibi yangu anapika
Hatta halafu kikesha
Chakula, tukajilia,
Yote nimeyandikia.
Wakatabahu harufu

339-343

Wakatabahu: kuandika
Ushairi umekwisha
Khabari ya Makunganya
Iliyo kujiri Kilwa
Nimekwisha kwambia.

344-348

Mwenyi kuandika usha'iri
Ana mu'alimu Mzee
Bin mu'allimu Ali
Bin Kidogo bin Al-Qadiri
Na il usuli Zingibari.